1 Mambo ya Nyakati 13

Sanduku la agano lasimamishwa Kiriath-yearimu

1 Daudi alishauriana na makamanda wa vikosi vya maelfu na vikosi vya mamia, pamoja na viongozi wote.

2 Kisha akawaambia Waisraeli wote waliokusanyika, “Ikiwa mtakubaliana nami, na ikiwa ni mapenzi yake Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, na tufanye hivi: Tutume wajumbe waende wakawaite ndugu zetu waliobaki nchini Israeli, pamoja na makuhani na Walawi walioko katika miji yao na malisho yao, waje wajumuike pamoja nasi.

3 Kisha twende tukalichukue sanduku la agano la Mungu wetu, maana hatukulijali wakati wa utawala wa mfalme Shauli.”

4 Watu wote walikubaliana na pendekezo hilo kwani waliliona kuwa jambo jema.

5 Hivyo, Daudi aliwakusanya Waisraeli wote nchini; toka kijito cha Shihori kilichoko Misri, hadi maingilio ya Hamathi ili kulileta sanduku la Mungu toka Kiriath-yearimu.

6 Daudi, akiandamana na Waisraeli wote, akaenda hadi mjini Baala, yaani Kiriath-yearimu, nchini Yudea, ili kulichukua toka huko sanduku la Mungu linaloitwa kwa jina lake Mwenyezi-Mungu akaaye kwenye kiti chake cha enzi juu ya viumbe vyenye mabawa.

7 Basi, wakalichukua sanduku la Mungu kutoka katika nyumba ya Abinadabu kwa gari jipya. Uza na Ahio waliliendesha gari hilo.

8 Daudi na Waisraeli wote wakawa wanacheza kwa nguvu zao zote, mbele ya Mungu. Waliimba huku wanapiga ala za muziki zilizotengenezwa kwa mvinje: Vinubi, vinanda, matari, matoazi na tarumbeta.

9 Walipofika kwenye uwanja wa kupuria nafaka wa Kidoni, Uza aliunyosha mkono wake kulishikilia sanduku la agano kwa sababu ng’ombe walijikwaa.

10 Mara Mwenyezi-Mungu akamkasirikia Uza kwa kulishika sanduku, akamuua. Uza akafa papo hapo mbele ya Mungu.

11 Daudi alikasirika kwa sababu Mwenyezi-Mungu alimuua Uza akiwa na hasira. Kwa sababu hiyo, mahali hapo huitwa Peres-uzahadi leo.

12 Siku hiyo Daudi akamwogopa Mungu, akasema, “Sasa, nitawezaje kulichukua sanduku la Mungu nyumbani mwangu?”

13 Basi, Daudi hakulichukua sanduku mpaka mji wa Daudi,bali alilipeleka nyumbani kwa Obed-edomu, Mgiti.

14 Sanduku hilo la Mungu lilikaa huko kwa Obed-edomu kwa muda wa miezi mitatu, naye Mwenyezi-Mungu akaibariki nyumba ya Obed-edomu na mali yake yote.