Isaya 13

Mungu ataiadhibu Babuloni

1 Kauli ya Mungu dhidi ya Babuloni ambayo Isaya, mwana wa Amozi, alipewa katika maono:

2 Mungu asema:

“Twekeni bendera juu ya mlima usio na miti.

Wapaazieni sauti askari

wapungieni watu mkono

waingie malango ya mji wa wakuu.

3 Mimi nimewaamuru wateule wangu,

nimewaita mashujaa wangu,

hao wenye kunitukuza wakishangilia,

waje kutekeleza lengo la hasira yangu.”

4 Sikilizeni kelele milimani

kama za kundi kubwa la watu!

Sikilizeni kelele za falme,

na mataifa yanayokusanyika!

Mwenyezi-Mungu wa majeshi

analikagua jeshi linalokwenda vitani.

5 Wanakuja kutoka nchi za mbali,

wanatoka hata miisho ya dunia:

Mwenyezi-Mungu na silaha za hasira yake

anakuja kuiangamiza dunia.

6 Lieni maana siku ya Mwenyezi-Mungu imekaribia;

inakuja kama maafa kutoka kwa Mungu Mwenye Nguvu.

7 Kwa hiyo mikono ya kila mtu italegea,

kila mtu atakufa moyo.

8 Watu watafadhaika,

watashikwa na hofu na maumivu,

watakuwa na uchungu kama mama anayejifungua.

Watatazamana kwa mashaka,

nyuso zao zitawaiva kwa haya.

9 Siku ya Mwenyezi-Mungu inakuja,

siku kali, ya ghadhabu na hasira kali.

Itaifanya nchi kuwa uharibifu,

itawaangamiza wenye dhambi wake.

10 Nyota na vilimia vyake angani hazitaangaza;

jua linapochomoza litakuwa giza,

na mwezi hautatoa mwanga wake.

11 Mwenyezi-Mungu asema hivi:

“Nitauadhibu ulimwengu kwa uovu wake,

waovu kwa sababu ya makosa yao.

Nitakikomesha kiburi cha wenye majivuno,

na kuporomosha ubaradhuli wa watu katili.

12 Nitawafanya watu kuwa wachache kuliko dhahabu safi;

binadamu watakuwa wachache kuliko dhahabu ya Ofiri.

13 Nitazitetemesha mbingu

nayo nchi itatikisika katika misingi yake

kwa sababu ya ghadhabu yangu Mwenyezi-Mungu

siku ile ya hasira yangu kali.

14 “Kama swala anayewindwa,

kama kondoo wasio na mchungaji,

kila mmoja atajiunga na watu wake

kila mtu atakimbilia nchini mwake.

15 Yeyote atakayeonekana atatumbuliwa,

atakayekamatwa atauawa kwa upanga.

16 Watoto wao wachanga watapondwapondwa mbele yao,

watanyanganywa nyumba zao,

na wake zao watanajisiwa.

17 “Ninawachochea Wamedi dhidi yao;

watu ambao hawajali fedha

wala hawavutiwi na dhahabu.

18 Mishale yao itawaua vijana,

hawatakuwa na huruma kwa watoto,

wala kuwahurumia watoto wachanga.

19 Babuloni johari ya falme zote

na umaarufu wa kiburi cha Wakaldayo

utakuwa kama Sodoma na Gomora,

wakati Mungu alipoiangamiza.

20 Kamwe hautakaliwa tena na watu,

watu hawataishi humo katika vizazi vyote.

Hakuna Mwarabu atakayepiga hema lake humo,

wala mchungaji atakayechunga wanyama wake humo.

21 Badala yake watakuwamo wanyama wakali wa porini,

bundi watajaa katika nyumba zake.

Mbuniwataishi humo,

na majiniyatachezea humo.

22 Mbwamwitu watalia ndani ya ngome zake,

mbweha wataonekana ndani ya nyumba zao za anasa.

Wakati wa Babuloni umekaribia,

wala siku zake hazitaongezwa.”