Mungu ataiangamiza Moabu
1 Kauli ya Mungu dhidi ya nchi ya Moabu.
Mji wa Ari nchini Moabu umeangamizwa usiku;
mji wa Kirinchini Moabu umeteketezwa usiku.
2 Watu wa Diboni wamepanda hekaluni, hadi mahali pa juu kuomboleza,
watu wa Moabu wanalia kwa ajili ya Nebo na Medeba;
vichwa vyote vimenyolewa upara,
ndevu zao zote zimekatwa kabisa.
3 Wanapita njiani wamevaa mavazi ya gunia.
Kwenye paa za nyumba na viwanja vya mji
watu wanalia na kukauka kwa machozi.
4 Watu wa Heshboni na Eleale wanalia,
sauti zao zinasikika hadi Yahazi.
Hata askari wa Moabu wanalia kwa sauti;
mioyo yao inatetemeka.
5 Moyo wangu unasononeka juu ya nchi ya Moabu;
wakimbizi wake wanakimbilia Soari,
wanakimbia mpaka Eglath-shelishiya.
Wanapanda njia ya kwenda Luhithi wakilia,
njiani kwenda Horonaimu wanatoa kilio cha maangamizi.
6 Kijito cha Nimrimu kimekauka;
nyasi zimekauka, majani mabichi yamenyauka,
hakuna chochote kinachoota hapo.
7 Watu wanavuka kijito cha Mierebi
wamebeba mali yao yote waliyochuma,
na kila walichojiwekea kama akiba.
8 Kilio kimezuka pote nchini Moabu,
maombolezo yao yamefika Eglaimu,
naam, yamefika mpaka Beer-elimu.
9 Maji ya Diboni yamejaa damu,
lakini Mungu ataongeza msiba wa Diboni.
Hao wachache watakaobaki hai
na kukimbia kutoka nchini Moabu,
watapelekewa simba wa kuwaua.