Isaya 23

Angamizo la Tiro na Sidoni

1 Kauli ya Mungu dhidi ya Tiro.

Ombolezeni, enyi mabaharia wa mbali baharini,

maana Tiro mji wenu umeharibiwa,

humo hamna tena makao wala bandari.

Mtazipokea habari hizo mtakaporejea kutoka Kupro.

2 Nyamazeni kwa mshangao enyi wakazi wa pwani,

naam, tulieni enyi wafanyabiashara wa Sidoni,

ambao wajumbe wenu wanapita baharini,

3 wakasafiri katika bahari nyingi.

Mapato yenu yalikuwa nafaka ya Misri,

mkaweza kufanya biashara na mataifa.

4 Aibu kwako ewe Sidoni,

mji wa ngome kando ya bahari!

Bahari yenyewe yatangaza:

“Sijapata kuwa na uchungu wa kuzaa,

wala sijawahi kuzaa;

sijawahi kulea wavulana,

wala kutunza wasichana!”

5 Habari zitakapoifikia Misri

kwamba Tiro imeangamizwa,

Wamisri watafadhaika sana.

6 Ombolezeni enyi wenyeji wa Foinike!

Jaribuni kukimbilia Tarshishi.

7 Je, huu ndio mji wa furaha wa Tiro,

mji ambao ulijengwa zamani za kale,

ambao wakazi wake walikwenda kumiliki nchi za mbali?

8 Ni nani aliyepanga mambo haya dhidi ya Tiro,

mji uliowatawaza wafalme,

wafanyabiashara wake walikuwa wakuu,

wakaheshimiwa duniani kote?

9 Ni Mwenyezi-Mungu wa majeshi!

Yeye ndiye aliyeyapanga haya yote.

Alifanya hivyo akiharibu kiburi chao

na kuwaaibisha waheshimiwa wake.

10 Limeni sasa ardhi yenu enyi wakazi wa Tarshishi;

maana hamna tena bandari kwa ajili ya meli kubwa.

11 Mwenyezi-Mungu ameunyosha mkono wake juu ya bahari,

amezitetemesha falme;

ametoa amri kuziharibu ngome za Kanaani.

12 Alisema: “Ewe binti Sidoni

hutaweza kufanya sherehe tena;

hata ukikimbilia Kupro,

huko nako hutapata pumziko!”

13 (Ni Wakaldayo, wala si Waashuru, waliowaacha wanyama wa porini wauvamie mji wa Tiro. Wao ndio waliouzungushia mji huo minara ya kuushambulia, wakayabomoa majumba yake na kuufanya magofu.)

14 Pigeni yowe enyi meli za Tarshishi,

maana kimbilio lenu limeharibiwa.

15 Hapo mji wa Tiro utasahaulika kwa muda wa miaka sabini, muda wa maisha ya mfalme. Baada ya miaka hiyo sabini, mji wa Tiro utakumbwa na kile watu wanachoimba juu ya malaya:

16 “Twaa kinubi chako

uzungukezunguke mjini,

ewe malaya uliyesahaulika!

Imba nyimbo tamutamu.

Imba nyimbo nyinginyingi

ili upate kukumbukwa tena.”

17 Baada ya miaka hiyo sabini, Mwenyezi-Mungu atauadhibu mji wa Tiro, nao utarudia kufanya uzinzi kwa kujiuza kwa mataifa yote ya dunia.

18 Fedha utakayopata itawekwa wakfu kwa Mwenyezi-Mungu. Mji wenyewe hautafaidika kwa fedha hiyo ila wale wanaomwabudu Mwenyezi-Mungu wataitumia kununulia chakula kingi na mavazi mazuri.