1 “Wewe Beli umeanguka;
Nebo umeporomoka.
Wakati mmoja watu walibeba sanamu zenu.
Sasa wanazibeba mgongoni mwa wanyama,
hao wanyama wachovu wamelemewa.
2 Nyinyi mmeanguka na kuvunjika,
hamwezi kuviokoa vinyago vyenu;
nyinyi wenyewe pia mtapelekwa uhamishoni!
3 “Sikilizeni enyi wazawa wa Yakobo,
nisikilizeni enyi mabaki ya watu wangu wa Israeli.
Mimi niliwatunzeni tangu mlipozaliwa;
niliwabebeni tangu tumboni mwa mama yenu.
4 Mimi ni yuleyule hata katika uzee wenu;
hata katika uzee wenu mimi nitawabeba.
Nilifanya hivyo kwanza,
nitafanya hivyo tena.
Nitawabeba nyinyi na kuwaokoa.
5 “Mtanifananisha na nani, tufanane?
Je, mwaweza kunilinganisha na nani, tulingane?
6 Watu humimina dhahabu kutoka mifuko yao,
hupima fedha kwenye mizani zao,
wakamwajiri mfua dhahabu atengeneze sanamu
kisha huisujudu na kuiabudu!
7 Hujitwisha sanamu hiyo mabegani, wakaibeba,
kisha huiweka mahali pake, ikakaa papo hapo;
kamwe haiwezi hata kusogea kutoka hapo ilipo.
Mtu akiililia, haiwezi kumwitikia,
wala haiwezi kumwokoa mtu katika taabu zake.
8 “Kumbukeni jambo hili na kutafakari,
liwazeni akilini mwenu enyi wakosefu.
9 Kumbukeni mambo niliyotenda hapo kale!
Mimi ndimi Mungu na hakuna mwingine;
naam, mimi ni Mungu, wala hakuna mwingine kama mimi.
10 Nilitangaza mambo ya mwisho tangu mwanzo,
tangu kale nilitangaza mambo yatakayotukia.
Lengo langu litatimia;
mimi nitatekeleza nia yangu yote.
11 Ninamwita tai wangu kutoka mashariki,
naam, msiri wangu kutoka nchi ya mbali.
Mimi nimenena na nitayafanya;
mimi nimepanga nami nitatekeleza.
12 “Nisikilizeni, enyi wenye vichwa vigumu,
nisikilizeni enyi mlio mbali na ukombozi.
13 Siku ya kuwakomboa naileta karibu,
haiko mbali tena;
siku ya kuwaokoeni haitachelewa.
Nitauokoa mji wa Siyoni,
kwa ajili ya Israeli, fahari yangu.