Mungu ataikomboa Yerusalemu
1 Amka! Amka!
Jipe nguvu zako ewe mji wa Siyoni!
Jivike mavazi yako mazuri,
ewe Yerusalemu, mji mtakatifu.
Maana hawataingia tena kwako
watu wasiotahiriwa na walio najisi.
2 Jikungute mavumbi, uinuke
ewe Yerusalemu uliyetekwa nyara!
Jifungue minyororo yako shingoni,
ewe binti Siyoni uliyechukuliwa mateka.
3 Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Nyinyi mliuzwa utumwani bila malipo yoyote, na mtakombolewa bila kulipa hata senti moja.
4 Tena mwanzoni nyinyi watu wangu mlikimbilia Misri mkakaa huko. Halafu baadaye Waashuru waliwakandamiza bila sababu yoyote.
5 Katika hali ya sasa napata faida gani kuwaona watu wangu wamepelekwa utumwani? Hao wanaowatawala wanajitapa. Nalo jina langu laendelea kudharauliwa kila siku.
6 Kwa hiyo watu wangu watajua mimi ni nani; siku hiyo watajua kwamba ni mimi ninayesema: Niko!”
7 Tazama inavyopendeza
kumwona mjumbe akitokea mlimani,
ambaye anatangaza amani,
ambaye analeta habari njema,
na kutangaza ukombozi!
Anauambia mji wa Siyoni:
“Mungu wako anatawala!”
8 Sikiliza sauti ya walinzi wako;
wanaimba pamoja kwa furaha,
maana wanaona kwa macho yao wenyewe,
kurudi kwa Mwenyezi-Mungu mjini Siyoni.
9 Pazeni sauti za shangwe, enyi magofu ya Yerusalemu!
Mwenyezi-Mungu amewafariji watu wake,
ameukomboa mji wa Yerusalemu.
10 Mwenyezi-Mungu ameonesha nguvu yake tukufu,
mbele ya mataifa yote.
Atawaokoa watu wake,
na ulimwengu wote utashuhudia.
11 Ondokeni! Ondokeni! Tokeni hapa;
msiguse kitu chochote najisi!
Ondokeni huku Babuloni!
Jitakaseni enyi mbebao vyombo vya Mwenyezi-Mungu.
12 Safari hii hamtatoka kwa haraka,
wala hamtaondoka mbiombio!
Maana Mwenyezi-Mungu atawatangulieni,
Mungu wa Israeli atawalinda kutoka nyuma.
Mtumishi wa Mwenyezi-Mungu
13 Mungu asema hivi:
“Mtumishi wangu atafanikiwa;
atatukuzwa na kupewa cheo,
atapata heshima kuu.
14 Wengi waliomwona walishtuka,
kwa vile sura yake ilikuwa imeharibiwa;
hakuwa tena na umbo la kibinadamu!
15 Lakini sasa ameyashangaza mataifa mengi.
Wafalme wanaduwaa kwa sababu yake,
maana wataona mambo ambayo hawajapata kuambiwa,
na kufahamu mambo ambayo hawajapata kusikia.”