Maombolezo 3

Adhabu, toba na tumaini

1 Mimi ni mtu niliyepata mateso

kwa fimbo ya ghadhabu yake Mungu.

2 Amenichukua akanipeleka

mpaka gizani kusiko na mwanga.

3 Amenyosha mkono wake dhidi yangu mimi tu,

akanichapa tena na tena mchana kutwa.

4 Amenichakaza ngozi na nyama,

mifupa yangu ameivunja.

5 Amenizingira na kunizungushia

uchungu na mateso.

6 Amenikalisha gizani

kama watu waliokufa zamani.

7 Amenizungushia ukuta nisitoroke,

amenifunga kwa minyororo mizito.

8 Ingawa naita na kulilia msaada

anaizuia sala yangu isimfikie.

9 Njia zangu ameziziba kwa mawe makubwa

amevipotosha vichochoro vyangu.

10 Yeye ni kama dubu anayenivizia;

ni kama simba aliyejificha.

11 Alinifukuza njiani mwangu,

akanilemaza na kuniacha mkiwa.

12 Aliuvuta upinde wake,

akanilenga mshale wake.

13 Alinichoma moyoni kwa mishale,

kutoka katika podo lake.

14 Nimekuwa kitu cha dhihaka kwa watu wote,

mchana kutwa nimekuwa mtu wa kuzomewa.

15 Amenijaza taabu,

akanishibisha uchungu.

16 Amenisagisha meno katika mawe,

akanifanya nigaegae majivuni.

17 Moyo wangu haujui tena amani,

kwangu furaha ni kitu kigeni.

18 Nimewaza “Nimekata tamaa kabisa,

tumaini langu kwa Mwenyezi-Mungu limetoweka.”

19 Kukumbuka taabu na kutangatanga kwangu

kwanipa uchungu kama wa nyongo.

20 Nayafikiria hayo daima,

nayo roho yangu imejaa majonzi.

21 Lakini nakumbuka jambo hili moja,

nami ninalo tumaini:

22 Kwamba fadhili za Mwenyezi-Mungu hazikomi,

huruma zake hazina mwisho.

23 Kila kunapokucha ni mpya kabisa,

uaminifu wake ni mkuu mno.

24 Mwenyezi-Mungu ndiye hazina yangu

hivyo nitamwekea tumaini langu.

25 Mwenyezi-Mungu ni mwema kwa wanaomtegemea,

ni mwema kwa wote wanaomtafuta.

26 Ni vema mtu kungojea kwa saburi

ukombozi utokao kwa Mwenyezi-Mungu.

27 Ni vema mtu kujifunza uvumilivu

tangu wakati wa ujana wake.

28 Heri kukaa peke na kimya,

mazito yanapompata kutoka kwa Mungu.

29 Yampasa kuinama na kujinyenyekesha,

huenda ikawa tumaini bado lipo.

30 Yampasa kumgeuzia shavu mwenye kumpiga,

na kuwa tayari kupokea matusi yake.

31 Mwenyezi-Mungu hatatutupa milele.

32 Ingawa atufanya tuhuzunike,

atakuwa na huruma tena

kadiri ya wingi wa fadhili zake.

33 Yeye hapendelei kuwatesa

wala kuwahuzunisha wanadamu.

34 Wafungwa wote nchini

wanapodhulumiwa na kupondwa;

35 haki za binadamu zinapopotoshwa

mbele yake Mungu Mkuu,

36 kesi ya mtu inapopotoshwa mahakamani,

je, Mwenyezi-Mungu haoni hayo?

37 Nani awezaye kuamuru kitu kifanyike

Mwenyezi-Mungu asipopanga iwe hivyo?

38 Maafa na mema hutokea tu

kwa amri yake Mungu Mkuu.

39 Kwa nini mtu anung’unike,

ikiwa ameadhibiwa kwa dhambi zake?

40 Na tupime na kuchunguza mwenendo wetu,

tupate kumrudia Mwenyezi-Mungu.

41 Tumfungulie Mungu huko mbinguni

mioyo yetu na kumwomba:

42 “Sisi tulikukosea na kukuasi

nawe bado hujatusamehe.

43 “Umejizungushia hasira yako ukatufuatia,

ukatuua bila huruma.

44 Umejizungushia wingu zito,

sala yeyote isiweze kupenya humo.

45 Umetufanya kuwa takataka na uchafu

miongoni mwa watu wa mataifa.

46 “Maadui zetu wote wanatuzomea.

47 Kitisho na hofu vimetuandama,

tumepatwa na maafa na maangamizi.

48 Macho yangu yabubujika mito ya machozi

kwa sababu ya kuangamizwa kwa watu wangu.

49 “Machozi yatanitoka bila kikomo,

50 mpaka Mwenyezi-Mungu kutoka huko mbinguni

aangalie chini na kuona.

51 Nalia na kujaa majonzi,

kuona yaliyowapata kina mama wa mji wangu.

52 “Nimewindwa kama ndege

na hao wanichukiao bila sababu.

53 Walinitupa shimoni nikiwa hai

na juu yangu wakarundika mawe.

54 Maji yalianza kunifunika kichwa,

nami nikafikiri, ‘Huu ni mwisho wangu.’

55 “Kutoka chini shimoni

nilikulilia ee Mwenyezi-Mungu.

56 Wewe umenisikia nikikulilia:

‘Usiache kusikia kilio changu cha msaada

bali unipatie nafuu.’

57 Nilipokuita ulinijia karibu

ukaniambia, ‘Usiogope!’

58 “Umenitetea katika kisa changu ee Mwenyezi-Mungu,

umeyakomboa maisha yangu.

59 Umeuona uovu niliotendewa ee Mwenyezi-Mungu,

uniamulie kwa wema kisa changu.

60 Umeuona uovu wa maadui zangu,

na mipango yao yote ya hila dhidi yangu.

61 “Umesikia matukano yao ee Mwenyezi-Mungu,

na mipango yao yote ya hila dhidi yangu.

62 Maneno na mawazo ya maadui zangu siku nzima

ni juu ya kuniangamiza mimi.

63 Wakati wote, wamekaa au wanakwenda,

mimi ndiye wanayemzomea.

64 Uwalipize, ee Mwenyezi-Mungu

kadiri ya hayo matendo yao,

kadiri ya mambo waliyotenda wenyewe.

65 Uipumbaze mioyo yao,

na laana yako iwashukie.

66 Uwafuatie kwa hasira, uwaangamize,

uwafanye watoweke ulimwenguni.”