Watu wanaungama dhambi zao
1 Siku ya ishirini na nne ya mwezi huo wa saba, watu wa Israeli walikusanyika, wakifunga na kuvaa mavazi ya magunia na kujipaka udongo kichwani kuonesha majuto yao.
2 Wakati huo, walikuwa wamejitenga mbali na watu wa mataifa mengine, wakasimama na kuungama dhambi zao na maovu ya babu zao.
3 Kwa muda wa kama masaa matatu, walisimama huku sheria ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, inasomwa. Na kwa masaa matatu yaliyofuata, walikuwa wakitubu na kumwabudu Mwenyezi-Mungu, Mungu wao.
4 Kuliwekwa jukwaa la Walawi; hapo walisimama Yeshua, Bani, Kadmieli, Shebania, Buni, Sherebia, Bani na Kenani. Wakamwomba kwa sauti kubwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wao.
5 Walawi, yaani: Yeshua, Kadmieli, Bani, Hashabuea, Sherebia, Hodia, Shebania na Pethahia wakawaambia watu;
“Simameni na kumsifu Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.
Msifuni milele na milele!
Na watu walisifu jina lako tukufu,
ambalo hutukuka kuliko baraka na sifa zote.”
Sala ya toba
6 Ezra akaomba kwa sala ifuatayo:
“Wewe peke yako ndiwe Mwenyezi-Mungu;
ndiwe uliyefanya mbingu na jeshi lake lote,
dunia na vyote vilivyomo,
bahari na vyote vilivyomo;
nawe ndiwe unayevihifadhi hai,
na jeshi lote la mbinguni lakuabudu wewe.
7 Wewe ndiwe Mwenyezi-Mungu,
Mungu uliyemchagua Abramu,
ukamtoa toka Uri ya Wakaldayo
na kumpa jina Abrahamu.
8 Ukamwona kuwa yu mwadilifu mbele yako;
ukafanya agano naye kuwapa wazawa wake nchi ya Wakanaani,
Wahiti, Waamori, Waperizi, Wayebusi na Wagirgashi.
Na ahadi yako ukaitimiza;
kwani wewe u mwaminifu.
9 “Uliyaona mateso ya babu zetu
walipokuwa nchini Misri,
na walipokuomba msaada kwenye Bahari ya Shamu
uliwasikia.
10 Ulifanya ishara na maajabu dhidi ya Farao,
watumishi wake wote
na watu wote wa nchi yake;
kwani ulijua kuwa
waliwakandamiza babu zetu.
Ukajipatia umaarufu uliopo mpaka leo.
11 Uliigawa bahari katikati mbele yao,
nao wakapita katikati ya bahari,
mahali pakavu.
Lakini ukawatupa Wamisri waliowafuatia
kama jiwe zito ndani ya maji mengi.
12 Mchana uliwaongoza kwa mnara wa wingu,
na usiku uliwaongoza kwa mnara wa moto
ili kuwamulikia njia ya kuendea.
13 Kule mlimani Sinai
ulishuka toka mbinguni na kuzungumza nao.
Ukawapa maagizo safi, sheria za kweli,
kanuni nzuri na amri.
14 Kwa njia ya Mose, mtumishi wako,
ukawajulisha Sabato yako takatifu
na ukawaagiza kuzifuata amri,
kanuni na sheria ulizowaamrisha.
15 Walipokuwa na njaa,
ukawapa chakula kutoka mbinguni.
Walipokuwa na kiu
ukawapa maji kutoka kwenye mwamba.
Ukawaagiza kuichukua nchi uliyokuwa umewaahidi.
16 Lakini wao na babu zetu wakawa na kiburi
na wakawa na shingo ngumu
wakakataa kufuata maagizo yako.
17 Wakakataa kutii;
wasiyakumbuke maajabu uliyofanya miongoni mwao.
Wakawa na shingo zao ngumu,
wakajichagulia kiongozi wa kuwarudisha
utumwani nchini Misri.
Bali wewe Mungu u mwepesi kusamehe,
mwenye neema na huruma,
wewe hukasiriki upesi.
U mwenye fadhili nyingi, na hukuwatupa.
18 Hata walipojitengenezea sanamu ya ndama na kusema,
‘Huyu ndiye mungu wetu
aliyetutoa kutoka nchi ya Misri,’
wakawa wamefanya kufuru kubwa.
19 Wewe kwa huruma zako nyingi
hukuwatupa kule jangwani.
Mnara wa wingu
uliowaongoza mchana haukuondoka,
wala mnara wa moto
uliowamulikia njia usiku, haukuondoka.
20 Ukawapa roho yako njema kuwashauri;
ukawapa mana kuwa chakula chao na maji ya kunywa
ili kutuliza kiu chao.
21 Ukawatunza jangwani kwa miaka arubaini
na hawakukosa chochote;
mavazi yao hayakuchakaa
wala nyayo zao hazikuvimba.
22 “Ukawaruhusu kushinda falme na mataifa,
ukawafanyia mengi kila upande.
Wakaishinda nchi ya Heshboni
alikotawala mfalme Sihoni;
na tena wakaishinda nchi ya Bashani
alikotawala mfalme Ogu.
23 Wazawa wao ukawafanya wawe wengi
kama nyota za mbinguni;
ukawaleta katika nchi
uliyowaahidi babu zao.
24 Hivyo, hao wazawa wakaja na kuimiliki nchi;
uliwashinda wakazi wa nchi hiyo,
Wakanaani, ukawatia mikononi mwao,
pamoja na wafalme wao,
watu wao na nchi yao ili wawatende wapendavyo.
25 Miji yenye ngome wakaiteka,
wakachukua nchi yenye utajiri,
majumba yenye vitu vingi vizuri,
visima vilivyochimbwa,
mashamba ya mizabibu na mizeituni
pamoja na miti yenye matunda kwa wingi.
Hivyo wakala,
wakashiba na kunenepa
na kuufurahia wema wako.
26 Lakini hawakuwa waaminifu kwako.
Wakakuasi,
wakaiacha sheria yako
na kuwaua manabii waliowaonya
ili wakurudie wewe.
Wakakufuru sana.
27 Hivyo, ukawatia katika mikono ya adui zao,
nao wakawatesa.
Lakini wakiwa katika mateso yao,
wakakulilia, nawe ukawasikia kutoka mbinguni.
Na kwa huruma zako nyingi,
ukawapelekea viongozi wa kuwaokoa;
nao wakawakomboa toka mikononi mwao.
28 Lakini amani ilipopatikana
wakatenda dhambi tena mbele yako,
nawe ukawaacha watiwe katika
mikono ya adui zao wawatawale.
Hata hivyo, walipotubu na kukulilia
ukawasikiliza kutoka mbinguni.
Na kwa kulingana na huruma zako nyingi,
ukawaokoa mara nyingi.
29 Ukawaonya ili wairudie sheria yako.
Hata hivyo, kwa kiburi chao,
wakaacha kuzitii amri zako.
Wakayaasi maagizo yako,
ambayo kwayo mtu akiyatii, ataishi.
Wakawa wajeuri
pia wakafanya shingo zao ngumu,
na wakakataa kuwa watiifu.
30 Ukawavumilia kwa miaka mingi,
na kuwaonya kwa njia ya roho yako
kwa kupitia manabii wako;
hata hivyo hawakusikiliza.
Basi ukawaacha
ukawatia mikononi mwa mataifa mengine.
31 Hata hivyo,
kutokana na huruma zako nyingi,
hukuwaacha waangamie kabisa au kuwatupa,
kwani wewe u Mungu mwenye neema
na huruma.
32 Kwa hiyo, ee Mungu wetu,
Mungu Mkuu,
mwenye nguvu na wa kutisha,
wewe unalishika agano lako
na una fadhili nyingi.
Mateso yaliyotupata, sisi,
wafalme wetu, wakuu wetu,
makuhani wetu, manabii wetu,
babu zetu na watu wako wote
tangu wakati wa wafalme wa Ashuru mpaka leo,
usiyaone kuwa ni madogo.
33 Hata hivyo,
unayo haki kwa kutuadhibu hivyo;
kwani wewe umekuwa mwaminifu
ambapo sisi tumekuwa watenda maovu.
34 Wafalme wetu, wakuu wetu,
makuhani wetu na babu zetu
hawajaishika sheria yako
wala kujali amri yako
na maonyo yako uliyowapa.
35 Hawakukutumikia katika ufalme wao,
wala walipoyafurahia mema yako mengi uliyowajalia kwa wingi,
katika nchi kubwa na yenye rutuba uliyowapa
hawakuyaacha matendo yao maovu.
36 Na leo tumekuwa watumwa;
tu watumwa katika nchi uliyowapa babu zetu
wafurahie matunda na vipawa vyake vyema.
37 Kwa sababu ya dhambi zetu,
utajiri wa nchi hii
unawaendea wafalme uliowaleta kututawala.
Wanatutawala wapendavyo
hata na mifugo yetu
wanaitendea wapendavyo,
tumo katika dhiki kuu.”
Watu wanatia sahihi mapatano
38 Kutokana na haya yote yaliyotokea, sisi tunaweka agano imara na wakuu wetu kwa maandishi; Walawi na makuhani wanatia sahihi zao na mhuri wao.