Sefania 3

Hukumu ya Yerusalemu

1 Ole wake mji wa Yerusalemu,

mji mchafu, najisi na mdhalimu.

2 Hausikilizi onyo lolote,

wala haukubali kukosolewa.

Haukumtegemea Mwenyezi-Mungu kamwe,

wala kumkaribia Mungu wake.

3 Viongozi wake ni simba wangurumao,

mahakimu wake ni mbwamwitu wenye njaa jioni

wasioacha chochote mpaka asubuhi.

4 Manabii wake ni watu wasiojali na wadanganyifu.

Makuhani wake wamevitia unajisi vitu vitakatifu

na kuihalifu sheria kwa nguvu.

5 Lakini Mwenyezi-Mungu aliye mjini humo ni mwadilifu,

yeye hatendi jambo lolote baya.

Kila siku asubuhi hudhihirisha kauli yake,

naam, kila kunapopambazuka huitekeleza.

Lakini wahalifu hawana aibu hata kidogo.

6 Mwenyezi-Mungu asema:

“Nimeyafutilia mbali mataifa;

kuta zao za kujikinga ni magofu.

Barabara zao nimeziharibu,

na hamna apitaye humo.

Miji yao imekuwa mitupu,

bila watu, na bila wakazi.

7 Nilisema, ‘Hakika mji huu watanicha

na kukubali kukosolewa;

hautaacha kukumbuka mara hizo zote nilizowaadhibu.’

Lakini watu wake walizidisha tamaa zao

za kufanya matendo yao kuwa upotovu.

8 “Kwa hiyo ningojeni mimi Mwenyezi-Mungu,

ngoja siku nitakapoinuka kutoa mashtaka.

Nimeamua kuyakusanya mataifa na falme,

kuyamwagia ghadhabu yangu,

kadhalika na ukali wa hasira yangu.

Dunia yote itateketezwa

kwa moto wa ghadhabu yangu.

9 “Wakati huo nitaibadili lugha ya watu,

nitawawezesha kusema lugha adili

ili waniite mimi Mwenyezi-Mungu,

na kuniabudu kwa moyo mmoja.

10 Kutoka ng’ambo ya mito ya Kushi

watu wangu wanaoniomba ambao wametawanyika,

wataniletea sadaka yangu.

11 “Siku hiyo, haitakulazimu kuona aibu,

kutokana na matendo yako ya kuniasi,

maana nitawaondoa miongoni mwako

wale wanaojigamba na kujitukuza

nawe hutakuwa na kiburi tena katika mlima wangu mtakatifu.

12 Nitakuachia watu wapole na wanyenyekevu

ambao watakimbilia usalama kwangu mimi Mwenyezi-Mungu.

13 Waisraeli watakaobaki,

hawatatenda mabaya wala hawatasema uongo;

wala kwao hatapatikana mdanganyifu yeyote.

Watapata malisho na kulala

wala hakuna mtu atakayewatisha.”

Wimbo wa furaha

14 Imba kwa sauti, ewe Siyoni,

paza sauti ee Israeli.

Furahi na kushangilia kwa moyo wote, ewe Yerusalemu!

15 Mwenyezi-Mungu amekuondolea hukumu iliyokukabili,

amewageuzia mbali adui zako.

Mwenyezi-Mungu, mfalme wa Israeli yuko pamoja nawe

hutaogopa tena maafa.

16 Siku hiyo, mji wa Yerusalemu utaambiwa:

“Usiogope, ee Siyoni,

usilegee mikono.

17 Mwenyezi-Mungu, Mungu wako yu pamoja nawe

yeye ni shujaa anayekuletea ushindi.

Yeye atakufurahia kwa furaha kuu,

kwa upendo wake atakujalia uhai mpya.

Atakufurahia kwa wimbo wa sauti kubwa,

18 kama vile katika siku ya sikukuu.”

Mwenyezi-Mungu asema:

“Nitakuondolea maafa yako,

nawe hutahitaji kuona aibu kwa ajili yake.

19 Wakati huo, nitawaadhibu wote wanaokukandamiza.

Nitawaokoa vilema na kuwakusanya waliotupwa,

na kubadili aibu yao kuwa sifa

na fahari duniani kote.

20 Wakati huo nitawakusanya,

na kuwafanya mjulikane na kusifiwa,

miongoni mwa watu wote duniani

nitakapowarudishia hali yenu njema

nanyi muone kwa macho yenu wenyewe.

Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”