Tamko la Mwenyezi-Mungu juu ya Filistia
1 Neno la Mwenyezi-Mungu lililomjia nabii Yeremia kuhusu Wafilisti, kabla Farao hajaushambulia mji wa Gaza:
2 Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Tazama! Maji yanapanda kutoka kaskazini,
nayo yatakuwa mto uliofurika;
yataifunika nchi nzima na vyote vilivyomo,
mji na wakazi na wanaoishi humo.
Watu watalia,
wakazi wote wa nchi wataomboleza.
3 Watasikia mshindo wa kwato za farasi,
kelele za magari ya vita,
na vishindo vya magurudumu yao.
Kina baba watawasahau watoto wao,
mikono yao itakuwa imelegea mno.
4 Hiyo ni siku ya kuwaangamiza Wafilisti wote,
kukomesha msaada uliobakia kutoka Tiro na Sidoni.
Maana Mwenyezi-Mungu anawaangamiza Wafilisti,
watu waliosalia wa kisiwa cha Kaftori.
5 Watu wa Gaza wamenyoa upara kuomboleza;
mji wa Ashkeloni umeangamia.
Enyi watu wa Anakimu mliobaki
mpaka lini mtajikatakata kwa huzuni?
6 Ee upanga wa Mwenyezi-Mungu!
Utachukua muda gani ndipo utulie?
Ingia katika ala yako,
ukatulie na kunyamaa!
7 Lakini utawezaje kutulia,
hali Mwenyezi-Mungu ameupa kazi?
Ameuamuru ushambulie mji wa Ashkeloni
na watu wanaoishi pwani.”