Jibu la Bildadi
1 Kisha Bildadi, Mshuhi, akajibu:
2 “Mungu ni mwenye uwezo mkuu,
watu wote na wamche.
Yeye huweka amani mpaka juu kwake mbinguni.
3 Nani awezaye kuhesabu majeshi yake?
Ni nani asiyeangaziwa na mwanga wake?
4 Mtu awezaje basi, kuwa mwadilifu mbele ya Mungu?
Binadamu tu awezaje kujidai kuwa safi?
5 Kwake Mungu, hata mwezi haungai vya kutosha;
nyota nazo si safi mbele yake;
6 sembuse mtu ambaye ni mdudu,
binadamu ambaye ni buu tu!”