Wimbo wa sifa
(Zaburi ya shukrani)
1 Mshangilieni Mwenyezi-Mungu, enyi nchi zote!
2 Mwabuduni Mwenyezi-Mungu kwa furaha,
nendeni kwake mkiimba kwa shangwe!
3 Jueni kwamba Mwenyezi-Mungu ni Mungu.
Yeye ndiye aliyetuumba, nasi ni mali yake;
sisi ni watu wake, ni kondoo wa malisho yake.
4 Pitieni milango ya hekalu lake kwa shukrani,
ingieni katika nyua zake kwa sifa.
Mshukuruni na kulisifu jina lake.
5 Mwenyezi-Mungu ni mwema;
fadhili zake zadumu milele,
na uaminifu wake katika vizazi vyote.