Mwongozo mzuri wa mfalme
(Zaburi ya Daudi)
1 Utenzi wangu kuhusu uaminifu na haki;
ninauimba kwa heshima yako, ee Mwenyezi-Mungu.
2 Nitazingatia mwenendo usio na hatia.
Je, utakuja kwangu lini?
Nitaishi kwa unyofu nyumbani kwangu;
3 sitavumilia kamwe upuuzi.
Nayachukia matendo ya watu wapotovu,
mambo yao hayataambatana nami.
4 Upotovu wowote ule uwe mbali nami;
sitahusika kabisa na uovu.
5 Anayemsengenya jirani nitamfutilia mbali;
sitamvumilia mwenye majivuno na kiburi.
6 Nitawaangalia kwa wema watu walio waaminifu,
wapate kuishi pamoja nami.
Watu wanyofu ndio watakaonitumikia.
7 Mwongo yeyote hatakaa nyumbani mwangu;
hakuna msema uongo atakayekaa kwangu.
8 Siku kwa siku nitawaangamiza waovu wote nchini;
nitawaangamiza wabaya wote mjini mwa Mwenyezi-Mungu.