Sala katika taabu
(Sala ya mtu aliye katika shida na ambaye anamwekea Mwenyezi-Mungu malalamiko yake)
1 Usikie sala yangu, ee Mwenyezi-Mungu,
na kilio changu kikufikie.
2 Usijifiche mbali nami wakati wa taabu!
Unitegee sikio lako,
unijibu upesi wakati ninapokuomba!
3 Siku zangu zapita kama moshi;
mifupa yangu yaungua kama katika tanuri.
4 Nimepondwa moyoni kama nyasi na kunyauka;
sina hata hamu ya chakula.
5 Kutokana na kusononeka kwangu,
nimebaki mifupa na ngozi.
6 Nimekuwa kama ndege wa jangwani;
kama bundi kwenye mahame.
7 Ninalala macho wazi,
kama ndege mkiwa juu ya paa.
8 Mchana kutwa maadui zangu wananisimanga,
wanaonidhihaki hutumia jina langu kulaania.
9 Majivu yamekuwa chakula changu,
machozi nayachanganya na kinywaji changu,
10 kwa sababu ya ghadhabu na hasira yako,
maana umeniokota na kunitupilia mbali.
11 Maisha yangu ni kama kivuli cha jioni;
ninanyauka kama nyasi.
12 Lakini wewe, ee Mwenyezi-Mungu, watawala milele;
jina lako lakumbukwa vizazi vyote.
13 Wewe utainuka na kuurehemu mji wa Siyoni;
maana wakati umefika wa kuutendea mema;
wakati wake uliopangwa umefika.
14 Watumishi wako wanauthamini sana,
ujapokuwa magofu sasa;
wanauonea huruma,
ingawa umeharibika kabisa.
15 Mataifa yataliheshimu jina la Mwenyezi-Mungu;
wafalme wote duniani wataogopa utukufu wake.
16 Mwenyezi-Mungu ataijenga upya Siyoni,
na kuonekana alivyo mtukufu.
17 Ataikubali sala ya fukara;
wala hatayakataa maombi yao.
18 Andika jambo hili kwa ajili ya vizazi vijavyo;
watakaozaliwa baadaye wamsifu Mwenyezi-Mungu.
19 Kwamba aliangalia chini kutoka patakatifu pake juu,
Mwenyezi-Mungu aliangalia dunia kutoka mbinguni,
20 akasikia lalamiko la wafungwa;
akawaachilia huru waliohukumiwa kuuawa.
21 Hivyo watu watatangaza jina la Mwenyezi-Mungu huko Siyoni;
sifa zake zitatangazwa huko Yerusalemu,
22 wakati mataifa yatakapokusanyika pamoja
na falme zitakutana kumwabudu Mwenyezi-Mungu.
23 Mungu amenipunguzia nguvu ningali kijana;
ameyafupisha maisha yangu.
24 Ee Mungu wangu, usinichukue sasa
wakati ningali bado kijana.
Ee Mwenyezi-Mungu wewe wadumu milele.
25 Wewe uliiumba dunia zamani za kale,
mbingu ni kazi ya mikono yako.
26 Hizo zitatoweka, lakini wewe wabaki;
hizo zitachakaa kama vazi.
Utazitupilia mbali kama nguo,
nazo zitapotelea mbali.
27 Lakini wewe ni yuleyule daima,
na maisha yako hayana mwisho.
28 Watoto wa watumishi wako watakaa salama;
wazawa wao wataimarishwa mbele yako.