Zaburi 11

Kumtumainia Mungu

(Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Daudi)

1 Kwake Mwenyezi-Mungu nakimbilia usalama;

mnawezaje basi kuniambia:

“Ruka kama ndege, mpaka milimani,

2 maana waovu wanavuta pinde;

wameweka mishale tayari juu ya uta,

wawapige mshale watu wema gizani!

3 Kama misingi ikiharibiwa,

mtu mwadilifu atafanya nini?”

4 Mwenyezi-Mungu yumo katika hekalu lake takatifu;

kiti cha enzi cha Mwenyezi-Mungu kiko mbinguni.

Kwa macho yake huwachungulia wanadamu,

na kujua kila kitu wanachofanya.

5 Mwenyezi-Mungu huwapima waadilifu na waovu;

huwachukia kabisa watu wakatili.

6 Atawanyeshea waovu makaa ya moto na madini ya kiberiti;

upepo wa hari utakuwa ndio adhabu yao.

7 Mwenyezi-Mungu ni mwadilifu na apenda uadilifu;

watu wanyofu watakaa pamoja naye.