Kutawazwa kwa mfalme mteule
(Zaburi ya Daudi)
1 Mwenyezi-Mungu amwambia bwana wangu:
“Keti upande wangu wa kulia,
hata niwaweke maadui zako chini ya miguu yako.”
2 Mwenyezi-Mungu ataeneza enzi yako kutoka Siyoni;
utatawala juu ya maadui zako wote.
3 Watu wako watakujia kwa hiari,
siku utakapokwenda kuwapiga maadui.
Juu ya milima mitakatifu watakujia vijana wako,
kama umande unaotokeza alfajiri mapema.
4 Mwenyezi-Mungu amekuapia wala hatabadili nia yake:
“Wewe ni kuhani milele kwa utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki.”
5 Bwana yuko upande wako wa kulia;
atawaponda wafalme atakapokasirika.
6 Atayahukumu mataifa na kuwaua watu wengi;
atawaponda viongozi kila mahali duniani.
7 Mfalme atakunywa maji ya kijito njiani;
naye atainua kichwa juu kwa ushindi.