Sifa kwa Mungu mtukufu
1 Msifuni Mwenyezi-Mungu!
Enyi watumishi wa Mwenyezi-Mungu, lisifuni jina lake!
2 Jina lake litukuzwe,
sasa na hata milele.
3 Kutoka mashariki na hata magharibi,
litukuzwe jina la Mwenyezi-Mungu!
4 Mwenyezi-Mungu atawala juu ya mataifa yote,
utukufu wake wafika juu ya mbingu.
5 Nani aliye kama Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu?
Yeye ameketi juu kabisa;
6 lakini anatazama chini,
azione mbingu na dunia.
7 Humwinua fukara kutoka mavumbini;
humnyanyua maskini kutoka unyonge wake,
8 na kumweka pamoja na wakuu;
pamoja na wakuu wa watu wake.
9 Humjalia mwanamke tasa furaha nyumbani kwake;
humfurahisha kwa kumjalia watoto.
Msifuni Mwenyezi-Mungu!