Mungu na watu wake
1 Watu wa Israeli walipotoka Misri,
wazawa wa Yakobo walipotoka ugenini,
2 Yuda ikawa maskani ya Mungu,
Israeli ikawa milki yake.
3 Bahari iliona hayo ikakimbia;
mto Yordani ukaacha kutiririka!
4 Milima ilirukaruka kama kondoo dume;
vilima vikaruka kama wanakondoo!
5 Ee bahari, imekuwaje hata ukakimbia?
Nawe Yordani, kwa nini ukaacha kutiririka?
6 Enyi milima, mbona mliruka kama kondoo dume?
Nanyi vilima, mmerukaje kama wanakondoo?
7 Tetemeka, ee dunia mbele yake Mwenyezi-Mungu;
tetemeka mbele ya Mungu wa Yakobo,
8 anayeugusa mwamba ukawa bwawa la maji,
nayo majabali yakawa chemchemi za maji!