Zaburi 115

Mungu mmoja wa kweli

1 Sio sisi, ee Mwenyezi-Mungu, sio sisi;

bali wewe peke yako utukuzwe,

kwa ajili ya fadhili zako na uaminifu wako.

2 Kwa nini mataifa yaseme:

“Mungu wenu yuko wapi?”

3 Mungu wetu yuko mbinguni;

yeye hufanya yote anayotaka.

4 Miungu yao ni ya fedha na dhahabu;

imetengenezwa kwa mikono ya wanadamu.

5 Ina vinywa, lakini haisemi.

Ina macho, lakini haioni.

6 Ina masikio, lakini haisikii.

Ina pua, lakini hainusi.

7 Ina mikono, lakini haipapasi.

Ina miguu, lakini haitembei.

Haiwezi kamwe kutoa sauti.

8 Wote wanaoitengeneza wanafanana nayo,

kadhalika na wote wanaoitumainia.

9 Enyi Waisraeli, mtumainieni Mwenyezi-Mungu;

yeye ndiye msaada wenu na ngao yenu.

10 Enyi wazawa wa Aroni, mtumainieni Mwenyezi-Mungu;

yeye ndiye msaada wenu na ngao yenu.

11 Enyi mnaomcha Mwenyezi-Mungu, mtumainini,

yeye ndiye msaada wenu na ngao yenu.

12 Mwenyezi-Mungu atukumbuka na atatubariki;

atawabariki watu wa Israeli,

atawabariki wazawa wa Aroni.

13 Atawabariki wote wamchao,

atawabariki wakubwa na wadogo.

14 Mwenyezi-Mungu awajalieni muongezeke;

awajalieni muongezeke nyinyi na wazawa wenu!

15 Mbarikiwe na Mwenyezi-Mungu,

aliyeziumba mbingu na dunia.

16 Mbingu ni mali yake Mwenyezi-Mungu,

bali dunia amewapa binadamu.

17 Wafu hawamsifu Mwenyezi-Mungu,

wala wale wanaoshuka katika nchi ya kimya.

18 Lakini sisi tulio hai twamsifu Mwenyezi-Mungu;

tutamsifu sasa na hata milele.

Msifuni Mwenyezi-Mungu!