Zaburi 116

Shukrani kwa kuokolewa kifoni

1 Nampenda Mwenyezi-Mungu,

kwa maana anisikia,

maana amesikia kilio cha ombi langu.

2 Yeye amenitegea sikio,

hivyo nitamwomba muda wote niishio.

3 Hatari ya kifo ilinizunguka,

vitisho vya kaburi vilinivamia;

nilijawa na mahangaiko na majonzi.

4 Kisha nikamlilia Mwenyezi-Mungu:

“Ee Mwenyezi-Mungu, tafadhali unisalimishe!”

5 Mwenyezi-Mungu amejaa wema na uaminifu;

Mungu wetu ni mwenye huruma.

6 Mwenyezi-Mungu huwalinda wanyofu;

nilipokuwa nimekandamizwa aliniokoa.

7 Uwe na utulivu mkuu, ee nafsi yangu,

maana Mwenyezi-Mungu amenitendea mema.

8 Ameniokoa kifoni na kufuta machozi yangu;

akanilinda nisije nikaanguka.

9 Nitatembea mbele yake Mwenyezi-Mungu,

katika nchi ya watu walio hai.

10 Nilikuwa na imani hata niliposema:

“Mimi nimetaabika mno.”

11 Hata nilisema kwa hofu yangu:

“Binadamu wote hawaaminiki!”

12 Nimrudishie nini Mwenyezi-Mungu,

kwa ukarimu wote alionitendea?

13 Nitamtolea tambiko ya divai kwa kunikomboa,

nitaomba kwa jina lake Mwenyezi-Mungu.

14 Nitamtimizia Mwenyezi-Mungu nadhiri zangu,

mbele ya watu wake wote.

15 Kifo cha waaminifu wake Mwenyezi-Mungu

si jambo dogo mbele yake.

16 Ee Mwenyezi-Mungu, mimi ni mtumishi wako;

ni mtumishi wako, mtoto wa mjakazi wako;

umenifungulia vifungo vyangu.

17 Nitakutolea tambiko za shukrani,

na kukupa heshima zangu.

18 Nitakutimizia ahadi zangu, ee Mwenyezi-Mungu

mbele ya watu wako wote,

19 waliokusanyika hekaluni mwako,

katikati ya Yerusalemu.

Msifuni Mwenyezi-Mungu!