Sala ya shukrani
1 Mshukuruni Mwenyezi-Mungu, kwa kuwa ni mwema,
kwa maana fadhili zake zadumu milele.
2 Watu wa Israeli na waseme:
“Fadhili zake zadumu milele.”
3 Wazawa wa Aroni na waseme:
“Fadhili zake zadumu milele.”
4 Wote wamchao Mwenyezi-Mungu na waseme:
“Fadhili zake zadumu milele.”
5 Katika taabu yangu nilimwomba Mwenyezi-Mungu,
naye akanisikia na kuniweka huru.
6 Mwenyezi-Mungu yuko nami, siogopi kitu;
binadamu ataweza kunifanya nini?
7 Mwenyezi-Mungu yuko nami, kunisaidia;
nami nitawaona maadui zangu wameshindwa.
8 Afadhali kukimbilia usalama kwa Mwenyezi-Mungu,
kuliko kumtumainia mwanadamu.
9 Afadhali kukimbilia usalama kwa Mwenyezi-Mungu,
kuliko kuwatumainia viongozi wa dunia.
10 Mataifa yote yalinizingira,
lakini kwa jina la Mwenyezi-Mungu nikayaangamiza!
11 Yalinizunguka kila upande,
lakini kwa jina la Mwenyezi-Mungu, nikayaangamiza!
12 Yalinizunguka, mengi kama nyuki,
lakini yakateketea kama kichaka motoni;
kwa jina la Mwenyezi-Mungu niliyaangamiza!
13 Nilishambuliwa mno karibu nishindwe,
lakini Mwenyezi-Mungu alinisaidia.
14 Mwenyezi-Mungu ni nguvu yangu kuu;
yeye mwenyewe ndiye wokovu wangu.
15 Sauti za furaha ya ushindi zasikika hemani mwao waadilifu:
“Mkono wa Mwenyezi-Mungu umetenda mambo makuu!
16 Mkono wa nguvu wa Mwenyezi-Mungu umeleta ushindi!
Mkono wa Mwenyezi-Mungu umetenda mambo makuu!”
17 Sitakufa, bali nitaishi,
na kusimulia matendo ya Mwenyezi-Mungu.
18 Mwenyezi-Mungu ameniadhibu sana,
lakini hakuniacha nife.
19 Nifungulie milango ya watu waadilifu,
niingie na kumshukuru Mwenyezi-Mungu!
20 Huu ndio mlango wa Mwenyezi-Mungu,
watu waadilifu watapitia humo.
21 Nakushukuru, ee Mungu kwa kunijibu;
kwa sababu wewe ni wokovu wangu.
22 Jiwe walilokataa waashi,
limekuwa jiwe kuu la msingi.
23 Hiyo ni kazi yake Mwenyezi-Mungu
nayo ni ya ajabu sana kwetu.
24 Hii ndiyo siku aliyoifanya Mwenyezi-Mungu;
tushangilie na kufurahi.
25 Tafadhali utuokoe, ee Mwenyezi-Mungu!
Tafadhali utufanikishe, ee Mwenyezi-Mungu!
26 Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Mwenyezi-Mungu!
Twawabariki kutoka nyumbani mwa Mwenyezi-Mungu
27 Mwenyezi-Mungu ni Mungu;
yeye ametujalia mwanga wake
Shikeni matawi ya sherehe,
mkiandamana mpaka madhabahuni.
28 Wewe ni Mungu wangu, nami ninakushukuru;
ninakutukuza, ee Mungu wangu.
29 Mshukuruni Mwenyezi-Mungu kwa kuwa ni mwema,
kwa maana fadhili zake zadumu milele.