Kuomba msaada
(Kwa Mwimbishaji: Mtindo wa Sheminithi. Zaburi ya Daudi)
1 Fanya haraka, ee Mwenyezi-Mungu!
Watu wema wamekwisha;
waaminifu wametoweka miongoni mwa watu.
2 Kila mmoja humdanganya mwenzake,
husema kwa kudanganya na kwa moyo wa unafiki.
3 Ee Mwenyezi-Mungu
uikomeshe hiyo midomo ya udanganyifu,
na ndimi hizo zinazojigamba kupindukia.
4 Wao husema: “Kwa ndimi zetu tutashinda;
midomo tunayo, nani awezaye kututawala?”
5 Lakini Mwenyezi-Mungu asema:
“Kwa sababu maskini wanadhulumiwa,
na wahitaji wanapiga kite, sasa naja,
nami nitawapa usalama wanaoutazamia.”
6 Neno la Mwenyezi-Mungu ni safi,
safi kama fedha iliyosafishwa katika tanuri,
naam, kama fedha iliyosafishwa mara saba.
7 Utulinde, ee Mwenyezi-Mungu,
utukinge daima na kizazi hiki kiovu.
8 Waovu wanazunguka kila mahali;
upotovu unatukuzwa kati ya watu.