Mungu kinga yetu
(Wimbo wa Kwenda Juu, wa Daudi)
1 Natazama juu milimani;
msaada wangu utatoka wapi?
2 Msaada wangu watoka kwa Mwenyezi-Mungu,
aliyeumba mbingu na dunia.
3 Hatakuacha uanguke;
mlinzi wako hasinzii.
4 Kweli mlinzi wa Israeli
hasinzii wala halali.
5 Mwenyezi-Mungu ni mlinzi wako;
yuko upande wako wa kulia kukukinga.
6 Mchana jua halitakuumiza,
wala mwezi wakati wa usiku.
7 Mwenyezi-Mungu atakukinga na baya lolote;
atayalinda salama maisha yako.
8 Mwenyezi-Mungu atakulinda katika shughuli zako zote
tangu sasa na hata milele.