Sifa za Yerusalemu
(Wimbo wa Kwenda Juu, wa Daudi)
1 Nilifurahi waliponiambia:
“Twende nyumbani kwa Mwenyezi-Mungu.”
2 Sasa tuko tumesimama,
kwenye malango yako, ee Yerusalemu!
3 Yerusalemu, mji uliojengwa,
ili jumuiya ikutane humo.
4 Humo ndimo makabila yanamofika,
naam, makabila ya Israeli,
kumshukuru Mwenyezi-Mungu kama alivyoagiza.
5 Humo mmewekwa mahakama ya hukumu ya haki,
mahakama ya ukoo wa kifalme wa Daudi.
6 Uombeeni Yerusalemu amani:
“Wote wakupendao na wafanikiwe!
7 Ndani ya kuta zako kuwe na amani,
majumbani mwako kuweko usalama!”
8 Kwa ajili ya jamaa na ndugu zangu,
ee Yerusalemu, nakutakia amani!
9 Kwa ajili ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu,
ninakuombea upate fanaka!