Zaburi 123

Kuomba huruma

(Wimbo wa Kwenda Juu)

1 Nakutazamia kwa hamu, ee Mwenyezi-Mungu,

nakuangalia wewe utawalaye huko juu mbinguni!

2 Kama watumishi wamtegemeavyo bwana wao,

kama mjakazi amtegemeavyo bibi yake,

ndivyo nasi tunavyokutegemea wewe,

ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu,

mpaka hapo utakapotuonea huruma.

3 Utuhurumie, ee Mwenyezi-Mungu, utuhurumie,

maana tumedharauliwa kupita kiasi.

4 Tumeshiba muda mrefu dharau za matajiri,

tumepuuzwa mno na wenye kiburi.