Mungu kinga yetu
(Wimbo wa Kwenda Juu, wa Daudi)
1 “Kama Mwenyezi-Mungu asingalikuwa upande wetu
Semeni nyote mlio katika Israeli:
2 “Kama Mwenyezi-Mungu asingalikuwa upande wetu,
wakati ule tuliposhambuliwa na maadui,
3 hakika tungalimezwa tukiwa hai,
wakati hasira zao zilipotuwakia.
4 Tungalikumbwa na gharika,
tungalifunikwa na mto wa maji,
5 mkondo wa maji ungalituchukua!”
6 Atukuzwe Mwenyezi-Mungu,
ambaye hakutuacha makuchani mwao.
7 Tumeponyoka kama ndege mtegoni;
mtego umeteguliwa, nasi tukaokoka.
8 Msaada wetu watoka kwa Mwenyezi-Mungu,
aliyeumba mbingu na dunia.