Bila Mungu kazi ya binadamu haifai
(Wimbo wa Kwenda Juu, wa Solomoni)
1 Mwenyezi-Mungu asipoijenga nyumba,
waijengao wanajisumbua bure.
Mwenyezi-Mungu asipoulinda mji,
waulindao wanakesha bure.
2 Mnajisumbua bure kuamka mapema asubuhi
na kuchelewa kwenda kupumzika jioni,
mjipatie chakula kwa jasho lenu.
Mungu huwaruzuku walio wake hata walalapo.
3 Watoto ni riziki kutoka kwa Mwenyezi-Mungu;
watoto ni tuzo lake kwetu sisi.
4 Watoto waliozaliwa wazazi wakiwa bado vijana,
ni kama mishale mikononi mwa askari.
5 Heri mtu aliye na mishale hiyo kwa wingi.
Hatashindwa atakapokabiliana na adui mahakamani.