Kuomba msaada
(Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Daudi)
1 Mpaka lini ee Mwenyezi-Mungu, utanisahau?
Je, utanisahau mpaka milele?
Mpaka lini utanificha uso wako?
2 Nitakuwa na wasiwasi rohoni hadi lini,
na sikitiko moyoni siku hata siku?
Hadi lini adui zangu watafurahia taabu zangu?
3 Uniangalie na kunijibu, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu.
Uyaangazie macho yangu, nisipatwe na usingizi wa kifo.
4 Usiwaache maadui zangu waseme: “Tumemweza huyu!”
Watesi wangu wasije wakafurahia kuanguka kwangu.
5 Lakini mimi nazitumainia fadhili zako;
moyo wangu na ufurahie wokovu wako.
6 Nitakuimbia wewe, ee Mwenyezi-Mungu,
kwa ukarimu mwingi ulionitendea!