Kuomba msaada
(Wimbo wa Kwenda Juu)
1 Toka upeo wa unyonge wangu,
nakulilia, ee Mwenyezi-Mungu.
2 Ee Bwana, sikia sauti yangu,
uitegee sikio sauti ya ombi langu.
3 Kama, ee Mwenyezi-Mungu ungekumbuka maovu yetu
nani, ee Bwana, angeweza kusalimika?
4 Lakini kwako twapata msamaha,
ili sisi tukuheshimu.
5 Namtumainia Mwenyezi-Mungu kwa moyo wangu wote;
nina imani sana na neno lake.
6 Ninamtumainia Mwenyezi-Mungu
kuliko walinzi wanavyongojea pambazuko;
kuliko walinzi wanavyongojea kuche asubuhi.
7 Ee Israeli, umtumainie Mwenyezi-Mungu,
maana kwake Mwenyezi-Mungu kuna fadhili,
kwake kuna nguvu kubwa ya kutukomboa.
8 Yeye atawakomboa watu wa Israeli
kutoka katika maovu yao yote.