Zaburi 132

Sifa ya nyumba ya Mungu

(Wimbo wa Kwenda Juu)

1 Ee Mwenyezi-Mungu, mkumbuke Daudi,

kumbuka taabu zote alizopata.

2 Ukumbuke ahadi aliyokupa, ee Mwenyezi-Mungu,

kiapo alichokuapia, ewe Mwenye Nguvu wa Yakobo:

3 “Sitaingia ndani ya nyumba yangu,

wala kulala kitandani mwangu;

4 sitakubali kulala usingizi,

wala kusinzia;

5 mpaka nikupatie wewe Mwenyezi-Mungu mahali pa kukaa,

makao yako, ewe Mwenye Nguvu wa Yakobo!”

6 Huko Efratha tulisikia habari za sanduku la agano,

tukalikuta katika mashamba ya Yearimu.

7 “Haya! Twende nyumbani kwa Mungu,

tuabudu mbele ya kiti chake cha enzi!”

8 Inuka ee Mwenyezi-Mungu, nenda kwenye maskani yako;

inuka pamoja na sanduku la agano la uwezo wako!

9 Makuhani wako wawe waadilifu daima;

na waaminifu wako wapige vigelegele vya furaha!

10 Kwa ajili ya Daudi, mtumishi wako,

usimkatae huyo mfalme uliyemweka wakfu.

11 Mwenyezi-Mungu alimwapia Daudi kiapo thabiti,

kiapo ambacho hatakibatilisha:

“Nitamtawaza mmoja wa wazawa wako mwenyewe,

kuwa mfalme baada yako.

12 Watoto wako wakishika agano langu,

na kuzingatia mafundisho nitakayowapa,

watoto wao pia watakuwa wafalme kama wewe.”

13 Mwenyezi-Mungu ameuchagua mji wa Siyoni,

ametaka uwe makao yake:

14 “Hapa ndipo nitakapokaa milele,

ndipo maskani yangu maana nimepachagua.

15 Nitaubariki sana mji wa Siyoni kwa mahitaji yake;

nitawashibisha chakula maskini wake.

16 Nitawafanikisha makuhani wake kwa wokovu;

waaminifu wake watapiga vigelegele vya furaha.

17 Humo nitamchipusha mfalme shujaa wa ukoo wa Daudi:

Kama taa iwakayo nitamtegemeza mfalme niliyemteua.

18 Maadui zake nitawavika aibu;

lakini yeye nitamvika fahari ya kifalme.”