Sifa kwa Mungu
1 Msifuni Mwenyezi-Mungu!
Lisifuni jina la Mwenyezi-Mungu,
msifuni enyi watumishi wake.
2 Msifuni enyi mkaao katika nyumba yake,
ukumbini mwa nyumba ya Mungu wetu!
3 Msifuni Mwenyezi-Mungu kwa kuwa ni mwema;
mtukuzeni kwa nyimbo maana inafaa.
4 Mwenyezi-Mungu amemchagua Yakobo kuwa wake,
nyinyi watu wa Israeli kuwa mali yake mwenyewe.
5 Najua hakika kuwa Mwenyezi-Mungu ni mkuu;
Bwana wetu ni mkuu juu ya miungu yote.
6 Mwenyezi-Mungu hufanya chochote anachotaka,
mbinguni, duniani, baharini na vilindini.
7 Ndiye aletaye mawingu kutoka mipaka ya dunia;
afanyaye gharika kuu kwa umeme,
na kuvumisha upepo kutoka ghala zake.
8 Ndiye aliyewaua wazaliwa wa kwanza huko Misri,
wazaliwa wa watu na wanyama kadhalika.
9 Ndiye aliyefanya ishara na maajabu kwako, ee Misri,
dhidi ya Farao na maofisa wake wote.
10 Ndiye aliyeyaangamiza mataifa mengi,
akawaua wafalme wenye nguvu:
11 Kina Sihoni mfalme wa Waamori,
Ogu mfalme wa Bashani,
na wafalme wote wa Kanaani.
12 Alichukua nchi zao na kuwapa watu wake;
naam, ziwe riziki ya watu wake Israeli.
13 Jina lako, ee Mwenyezi-Mungu, ladumu milele,
utakumbukwa kwa fahari nyakati zote.
14 Mwenyezi-Mungu atawatetea watu wake;
na kuwaonea huruma watumishi wake.
15 Miungu ya uongo ya mataifa ni fedha na dhahabu,
imetengenezwa kwa mikono ya binadamu.
16 Ina vinywa, lakini haisemi;
ina macho, lakini haioni.
17 Ina masikio, lakini haisikii;
wala haiwezi hata kuvuta pumzi.
18 Wote walioifanya wafanane nayo,
naam, kila mmoja anayeitegemea!
19 Enyi watu wa Israeli, mtukuzeni Mwenyezi-Mungu!
Enyi makuhani, mtukuzeni Mwenyezi-Mungu!
20 Enyi Walawi, mtukuzeni Mwenyezi-Mungu!
Enyi wachaji wa Mwenyezi-Mungu, mtukuzeni!
21 Atukuzwe Mwenyezi-Mungu katika Siyoni,
atukuzwe katika makao yake Yerusalemu.
Msifuni Mwenyezi-Mungu!