Zaburi 140

Sala ya kuomba ulinzi wa Mungu

(Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Daudi)

1 Ee Mwenyezi-Mungu, uniokoe na watu wabaya,

unikinge na watu wakatili.

2 Watu hao huwaza mabaya daima,

huzusha magomvi kila mara.

3 Ndimi zao hatari kama za nyoka;

midomoni mwao mna maneno ya sumu kama ya joka.

4 Ee Mwenyezi-Mungu, unilinde na makucha ya wabaya;

unikinge na watu wakatili

ambao wamepanga kuniangusha.

5 Wenye kiburi wamenitegea mitego,

wametandaza kamba kama wavu,

wameficha mitego njiani wanikamate.

6 Namwambia Mwenyezi-Mungu, “Wewe ndiwe Mungu wangu.”

Usikilize, ee Mwenyezi-Mungu, sauti ya ombi langu.

7 Ee Mwenyezi-Mungu, Bwana wangu, mkombozi wangu mkuu,

umenikinga salama wakati wa vita.

8 Ee Mwenyezi-Mungu, usiwape waovu wanayotaka;

wala mipango yao mibaya usiifanikishe.

9 Hao wanaonizingira wanainua vichwa;

uovu wa maneno yao uwapate wao wenyewe!

10 Makaa ya moto yawaangukie;

watumbukizwe mashimoni, wasiinuke tena.

11 Wanaowasengenya wengine wasifanikiwe katika nchi;

uovu uwapate wakatili na kuwaangamiza mara!

12 Najua Mwenyezi-Mungu hutetea kisa cha wanaoteswa,

na kuwapatia haki maskini.

13 Hakika waadilifu watalisifu jina lako;

wanyofu watakaa kwako.