Hatari za tamaa mbaya
(Zaburi ya Daudi)
1 Nakuita, ee Mwenyezi-Mungu,
uje haraka kunisaidia!
Uisikilize sauti yangu wakati ninapokuita!
2 Sala yangu uipokee kama ubani;
niinuapo mikono yangu kwako unikubali kama tambiko ya jioni.
3 Ee Mwenyezi-Mungu ukilinde kinywa changu,
uweke ulinzi mlangoni mwa mdomo wangu.
4 Unikinge nisielekee kufanya mabaya,
nisijishughulishe na matendo maovu;
nisijiunge na watu watendao mabaya,
wala nisishiriki kamwe karamu zao.
5 Afadhali mtu mwema anipige kunionya;
lakini sikubali kamwe kusifiwa na wabaya,
maana nasali daima dhidi ya maovu yao.
6 Wakuu wao watakapopondwa miambani,
ndipo watatambua maneno yangu yalikuwa sawa.
7 Mifupa yao itatawanywa mdomoni pa Kuzimu
kama kuni zilizopasuliwa vipandevipande!
8 Bali mimi nakutegemea, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu;
ninakimbilia usalama kwako, usiniache hatarini.
9 Unikinge na mitego waliyonitegea,
uniepushe na matanzi ya hao watu waovu.
10 Waovu wanaswe katika mitego yao wenyewe,
wakati mimi najiendea zangu salama.