Dua ya mtu aliyeachwa mpweke
(Utenzi wa Daudi alipokuwa pangoni. Sala)
1 Namlilia Mwenyezi-Mungu kwa sauti,
namsihi Mwenyezi-Mungu kwa sauti yangu.
2 Namwekea malalamiko yangu,
namweleza taabu zangu.
3 Ninapokaribia kukata tamaa kabisa,
yeye yupo, anajua mwenendo wangu.
Maadui wamenitegea mitego njiani mwangu.
4 Nikiangalia upande wa kulia na kungojea,
naona hakuna mtu wa kunisaidia;
sina tena mahali pa kukimbilia,
hakuna mtu anayenijali.
5 Nakulilia wewe, ee Mwenyezi-Mungu!
Wewe ni kimbilio langu la usalama;
wewe ni riziki yangu kuu katika nchi ya walio hai.
6 Usikilize kilio changu, maana nimekuwa hoi;
uniokoe na watesi wangu, maana wamenizidi nguvu.
7 Unitoe humu kifungoni,
ili nipate kukushukuru.
Watu waadilifu watajiunga nami
kwa sababu umenitendea mema mengi.