Sala ya kuomba msaada
(Zaburi ya Daudi)
1 Usikie sala yangu, ee Mwenyezi-Mungu!
Ulitegee sikio ombi langu
maana wewe ni mwaminifu;
unijibu kwa sababu ya uadilifu wako.
2 Usinitie hukumuni mimi mtumishi wako,
maana hakuna yeyote aliye mwadilifu mbele yako.
3 Maadui zangu wamenifuatia;
wameniangusha chini kabisa
wameniketisha gizani kama mtu aliyekufa zamani.
4 Nimevunjika moyo kabisa;
nimekufa ganzi kwa ajili ya woga.
5 Nakumbuka siku zilizopita;
natafakari juu ya yote uliyotenda,
nawaza na kuwazua juu ya matendo yako.
6 Nakunyoshea mikono yangu kuomba;
nina kiu yako kama nchi kavu isiyo na maji.
7 Ee Mwenyezi-Mungu, unijibu haraka;
maana nimekata tamaa kabisa!
Usijifiche mbali nami,
nisije nikawa kama wale washukao kwa wafu.
8 Asubuhi unioneshe fadhili zako,
maana nimekuwekea tumaini langu.
Unifundishe mwenendo wa kufuata,
maana nakuelekezea ombi la moyo wangu.
9 Uniokoe, ee Mwenyezi-Mungu, kutoka maadui zangu,
maana kwako nakimbilia usalama.
10 Unifundishe kutimiza matakwa yako,
maana wewe ni Mungu wangu!
Roho yako nzuri iniongoze katika njia sawa.
11 Unifadhili, ee Mwenyezi-Mungu, kwa hisani yako,
uniondoe katika taabu kwa sababu ya uadilifu wako.
12 Kwa sababu ya fadhili zako uwakomeshe maadui zangu,
uwaangamize wote wanaonidhulumu;
maana mimi ni mtumishi wako.