Sifa kwa Mungu Mwokozi
1 Msifuni Mwenyezi-Mungu!
Umsifu Mwenyezi-Mungu, ee nafsi yangu!
2 Nitamsifu Mwenyezi-Mungu maisha yangu yote;
nitamwimbia Mungu wangu muda wote niishipo.
3 Msiwategemee wakuu wa dunia;
hao ni binadamu tu, hawawezi kuokoa.
4 Binadamu akitoa pumzi yake ya mwisho,
anarudi mavumbini alimotoka;
na hapo mipango yake yote hutoweka.
5 Heri mtu anayesaidiwa na Mungu wa Yakobo,
mtu aliyeweka tumaini lake kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wake,
6 aliyeumba mbingu na dunia,
bahari na vyote vilivyomo.
Yeye hushika ahadi yake milele.
7 Yeye huwapatia wanaoonewa haki zao,
huwapa wenye njaa chakula.
Mwenyezi-Mungu huwapa wafungwa uhuru,
8 huwafungua macho vipofu.
Mwenyezi-Mungu huwainua waliokandamizwa;
huwapenda watu walio waadilifu.
9 Mwenyezi-Mungu huwalinda wageni,
huwategemeza wajane na yatima;
lakini huipotosha njia ya waovu.
10 Mwenyezi-Mungu atawala milele,
Mungu wako, ee Siyoni, ni mfalme vizazi vyote!
Msifuni Mwenyezi-Mungu!