Zaburi 149

Wimbo wa ushindi

1 Msifuni Mwenyezi-Mungu!

Mwimbieni Mwenyezi-Mungu wimbo mpya;

msifuni katika kusanyiko la waaminifu!

2 Furahi ee Israeli kwa sababu ya Muumba wako,

wakazi wa Siyoni shangilieni kwa sababu ya Mfalme wenu.

3 Lisifuni jina lake kwa ngoma,

mwimbieni kwa ngoma na zeze.

4 Maana Mwenyezi-Mungu hupendezwa na watu wake;

yeye huwapamba wanyonge kwa ushindi.

5 Watu waaminifu wafurahi kwa fahari;

washangilie hata walalapo.

6 Wabubujike sifa kuu za Mungu,

na panga zenye makali kuwili mikononi mwao,

7 wawalipe kisasi watu wa mataifa,

wawaadhibu watu wasiomjua Mungu;

8 wawafunge wafalme wao kwa minyororo,

na viongozi wao kwa pingu za chuma,

9 kusudi watekeleze adhabu iliyoamriwa!

Hiyo ndiyo fahari ya waaminifu wa Mungu.

Msifuni Mwenyezi-Mungu!