Rafiki ya Mungu
(Zaburi ya Daudi)
1 Nani ee Mwenyezi-Mungu atakayekaa hemani mwako?
Nani atakayeishi juu ya mlima wako mtakatifu?
2 Ni mtu aishiye bila lawama,
atendaye daima yaliyo mema,
asemaye ukweli kutoka moyoni;
3 ni mtu asiyesengenya watu,
asiyemtendea uovu rafiki yake,
wala kumfitini jirani yake;
4 ni mtu anayewadharau wafisadi,
lakini huwaheshimu wamchao Mwenyezi-Mungu;
ni mtu asiyegeuza kiapo chake hata kikimtia hasara;
5 asiyekopesha fedha yake kwa riba,
wala kupokea rushwa kumdhulumu asiye na hatia.
Mtu atendaye hayo,
kamwe hatatikisika.