Zaburi 150

Zaburi ya kumsifu Mungu

1 Msifuni Mwenyezi-Mungu!

Msifuni Mungu katika patakatifu pake;

msifuni katika mbingu zake kuu.

2 Msifuni kwa sababu ya matendo yake makuu;

msifuni kwa ajili ya utukufu wake mkuu.

3 Msifuni kwa mlio wa tarumbeta;

msifuni kwa zeze na kinubi!

4 Msifuni kwa ngoma na kucheza;

msifuni kwa filimbi na banjo!

5 Msifuni kwa kupiga matoazi.

Msifuni kwa matoazi ya sauti kubwa.

6 Kila kiumbe hai kimsifu Mwenyezi-Mungu!

Msifuni Mwenyezi-Mungu!