Zaburi 24

Mfalme Mkuu

(Zaburi ya Daudi)

1 Dunia na vyote vilivyomo ni vyake Mwenyezi-Mungu;

ulimwengu na wote waishio humo ni mali yake.

2 Maana yeye aliweka misingi ya dunia juu ya bahari;

aliisimika imara juu ya mito ya maji.

3 Nani atakayepanda mlima wa Mwenyezi-Mungu?

Nani atakayekaa katika hekalu lake takatifu?

4 Ni mtu wa matendo mema na moyo safi,

asiyeuelekeza moyo wake katika upuuzi,

wala kuapa kwa uongo.

5 Mtu huyo atapokea baraka kwa Mwenyezi-Mungu,

na haki yake kwa Mungu mwokozi wake.

6 Ndio hali ya kizazi cha watu wamtafutao yeye;

naam, watu wamtafutao Mungu wa Yakobo.

7 Fungukeni enyi milango;

fungukeni enyi milango ya kale,

ili Mfalme mtukufu aingie.

8 Ni nani huyo Mfalme mtukufu?

Ni Mwenyezi-Mungu, mwenye nguvu na uwezo;

Mwenyezi-Mungu, mwenye uwezo vitani.

9 Fungukeni enyi malango,

fungukeni enyi milango ya kale,

ili Mfalme mtukufu aingie.

10 Ni nani huyo Mfalme mtukufu?

Ni Mwenyezi-Mungu, wa majeshi,

yeye ndiye Mfalme mtukufu.