Kumwomba Mungu uongozi na ulinzi
(Zaburi ya Daudi)
1 Ee Mwenyezi-Mungu, kwako naielekeza nafsi yangu!
2 Nakutumainia wewe, ee Mungu wangu,
usiniache niaibike;
adui zangu wasifurahie kushindwa kwangu.
3 Usimwache anayekutumainia apate aibu;
lakini waaibike wote wanaokuasi kwa makusudi.
4 Unijulishe njia zako, ee Mwenyezi-Mungu;
unifundishe nifuate unayotaka.
5 Uniongoze katika ukweli wako na kunifundisha,
kwani wewe ni Mungu, mwokozi wangu;
ninakutegemea wewe kila siku.
6 Uikumbuke huruma yako ee Mwenyezi-Mungu;
uzikumbuke na fadhili zako kuu,
ambazo zimekuwako tangu kale.
7 Usikumbuke dhambi na makosa ya ujana wangu;
unikumbuke kadiri ya fadhili zako,
kwa ajili ya wema wako, ee Mwenyezi-Mungu.
8 Mwenyezi-Mungu ni mwema na mnyofu,
kwa hiyo huwafundisha wenye dhambi njia.
9 Huwaongoza wanyenyekevu katika uadilifu;
naam, huwafundisha hao njia yake.
10 Mwenyezi-Mungu hutenda kwa fadhili na uaminifu,
kwa wale wanaoshika agano lake na maamuzi yake.
11 Kwa ajili ya jina lako, ee Mwenyezi-Mungu,
unisamehe kosa langu kwani ni kubwa.
12 Kila mtu anayemcha Mwenyezi-Mungu,
Mwenyezi-Mungu atamfunza njia ya kufuata.
13 Mtu wa namna hiyo atafanikiwa daima,
na wazawa wake watamiliki nchi.
14 Mwenyezi-Mungu ni rafiki ya wale wamchao;
yeye huwajulisha hao agano lake.
15 Namwangalia Mwenyezi-Mungu daima;
yeye atainasua miguu yangu mtegoni.
16 Unielekee, ee Mungu, unionee huruma,
maana mimi ni mpweke na mnyonge.
17 Uniondolee mahangaiko ya moyoni mwangu;
unitoe katika mashaka yangu.
18 Uangalie mateso yangu na dhiki yangu;
unisamehe dhambi zangu zote.
19 Angalia jinsi walivyo wengi maadui zangu;
ona jinsi wanavyonichukia kwa ukatili.
20 Uyalinde maisha yangu, uniokoe;
nakimbilia usalama kwako,
usikubali niaibike.
21 Wema na uadilifu vinihifadhi,
maana ninakutumainia wewe.
22 Ee Mungu, uwaokoe watu wako, Israeli;
uwaokoe katika taabu zao zote.