Zaburi 26

Sala ya mtu mwema

(Zaburi ya Daudi)

1 Ee Mwenyezi-Mungu, unitetee,

maana nimeishi bila hatia,

nimekutumainia wewe bila kusita.

2 Unijaribu, ee Mwenyezi-Mungu, na kunipima;

uchunguze moyo wangu na akili zangu.

3 Fadhili zako ziko mbele ya macho yangu,

ninaishi kutokana na uaminifu wako.

4 Sijumuiki na watu wapotovu;

sishirikiani na watu wanafiki.

5 Nachukia mikutano ya wabaya;

wala sitajumuika na waovu.

6 Nanawa mikono yangu kuonesha sina hatia,

na kuizunguka madhabahu yako, ee Mwenyezi-Mungu,

7 nikiimba wimbo wa shukrani,

na kusimulia matendo yako yote ya ajabu.

8 Ee Mwenyezi-Mungu, napenda makao yako,

mahali unapokaa utukufu wako.

9 Usiniangamize pamoja na wenye dhambi,

wala usinitupe pamoja na wauaji,

10 watu ambao matendo yao ni maovu daima,

watu ambao wamejaa rushwa.

11 Lakini mimi ninaishi kwa unyofu;

unihurumie na kunikomboa.

12 Mimi nimesimama mahali palipo imara;

nitamsifu Mwenyezi-Mungu katika kusanyiko kubwa.