Sauti ya Mungu katika dhoruba
(Zaburi ya Daudi)
1 Mpeni Mwenyezi-Mungu heshima enyi viumbe vya mbinguni,
semeni Mwenyezi-Mungu ni mtukufu na mwenye nguvu.
2 Semeni jina la Mwenyezi-Mungu ni tukufu.
Mwabuduni katika mahali pake patakatifu.
3 Sauti ya Mwenyezi-Mungu yasikika juu ya maji;
Mungu mtukufu angurumisha radi,
sauti ya Mwenyezi-Mungu yasikika juu ya bahari!
4 Sauti ya Mwenyezi-Mungu ina nguvu,
sauti ya Mwenyezi-Mungu imejaa fahari.
5 Sauti ya Mwenyezi-Mungu huvunja mierezi;
Mwenyezi-Mungu avunja mierezi ya Lebanoni.
6 Huirusha milima ya Lebanoni kama ndama,
milima ya Sirionikama mwananyati.
7 Sauti ya Mwenyezi-Mungu hutoa miali ya moto.
8 Sauti ya Mwenyezi-Mungu hutetemesha jangwa,
Mwenyezi-Mungu hutetemesha jangwa la Kadeshi.
9 Sauti ya Mwenyezi-Mungu huitikisa mivule,
hukwanyua majani ya miti msituni,
na hekaluni mwake wote wasema:
“Utukufu kwa Mungu!”
10 Mwenyezi-Mungu ameketi juu ya gharika;
Mwenyezi-Mungu ni mfalme atawalaye milele.
11 Mwenyezi-Mungu na awape watu wake nguvu!
Mwenyezi-Mungu na awabariki watu wake kwa amani!