Sala ya shukrani
(Zaburi ya Daudi)
1 Ee Mwenyezi-Mungu, nakutukuza maana umeniokoa,
wala hukuwaacha maadui zangu wanisimange.
2 Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu,
nilikulilia msaada, nawe ukaniponya.
3 Ee Mwenyezi-Mungu, umeniokoa kutoka kuzimu;
umenipa tena uhai,
umenitoa miongoni mwa waendao kuzimu.
4 Mwimbieni Mwenyezi-Mungu sifa, enyi waaminifu wake;
kumbukeni utakatifu wake na kumshukuru.
5 Hasira yake hudumu kitambo kidogo,
wema wake hudumu milele.
Kilio chaweza kuwapo hata usiku,
lakini asubuhi huja furaha.
6 Mimi nilipofanikiwa, nilisema:
“Kamwe sitashindwa!”
7 Kwa wema wako, ee Mwenyezi-Mungu,
umeniimarisha kama mlima mkubwa.
Lakini ukajificha mbali nami,
nami nikafadhaika.
8 Nilikulilia wewe, ee Mwenyezi-Mungu;
naam niliomba dua kwako ee Mwenyezi-Mungu:
9 “Je, utapata faida gani nikifa
na kushuka hadi kwa wafu?
Je, mavumbi ya wafu yanaweza kukusifu?
Je, yanaweza kusimulia uaminifu wako?
10 Usikie, ee Mwenyezi-Mungu, unihurumie;
ee Mwenyezi-Mungu, unisaidie!”
11 Wewe umegeuza maombolezo langu kuwa ngoma ya furaha;
umeniondolea huzuni yangu, ukanizungushia furaha.
12 Mimi nitakusifu wala sitakaa kimya.
Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu nitakushukuru milele.