Zaburi 34

Sifa kwa wema wa Mungu

(Zaburi ya Daudi alipojifanya mwendawazimu mbele ya Abimeleki)

1 Nitamtukuza Mwenyezi-Mungu nyakati zote,

sitaacha kamwe kuzitamka sifa zake.

2 Mimi nitaona fahari juu ya Mwenyezi-Mungu,

wanyonge wasikie na kufurahi.

3 Mtukuzeni Mwenyezi-Mungu pamoja nami,

sote pamoja tulisifu jina lake.

4 Nilimwomba Mwenyezi-Mungu naye akanijibu,

na kuniondoa katika hofu zangu zote.

5 Mgeukieni Mungu mpate kufurahi;

nanyi hamtaaibishwa kamwe.

6 Maskini alimlilia Mwenyezi-Mungu, naye akamsikia,

na kumwokoa katika taabu zake zote.

7 Malaika wa Mwenyezi-Mungu huwalinda wote wamchao,

na kuwaokoa katika hatari.

8 Jaribuni mwone Mwenyezi-Mungu alivyo mwema.

Heri mtu anayekimbilia usalama kwake.

9 Mcheni Mwenyezi-Mungu enyi watakatifu wake;

maana wenye kumcha hawatindikiwi na kitu.

10 Hata wanasimba hutindikiwa na kuona njaa;

lakini wanaomtafuta Mwenyezi-Mungu hawakosi chochote chema.

11 Njoni enyi vijana mkanisikilize,

nami nitawafundisha kumcha Mwenyezi-Mungu.

12 Je, watamani kufurahia maisha,

kuishi maisha marefu na kufurahia mema?

13 Basi, acha kusema mabaya,

na kuepa kusema uongo.

14 Jiepushe na uovu, utende mema;

utafute amani na kuizingatia.

15 Mwenyezi-Mungu huwaangalia waadilifu,

na kusikiliza malalamiko yao;

16 lakini huwapinga watu watendao maovu,

awafutilie mbali kutoka duniani.

17 Waadilifu wakimlilia Mwenyezi-Mungu yeye huwasikia,

na kuwaokoa katika taabu zao zote.

18 Mwenyezi-Mungu yu karibu na waliokufa moyo;

huwaokoa wote waliokata tamaa kabisa.

19 Mateso ya mwadilifu ni mengi,

lakini Mwenyezi-Mungu humwokoa kutoka yote.

20 Huvilinda viungo vya mwili wake wote,

hakuna hata mfupa wake mmoja utakaovunjwa.

21 Ubaya huwaletea waovu kifo;

wanaowachukia waadilifu wataadhibiwa.

22 Mwenyezi-Mungu huokoa maisha ya watumishi wake,

wote wanaomkimbilia hawataadhibiwa.