Kuomba msaada jioni
(Kwa Mwimbishaji: Na ala za nyuzi za muziki. Zaburi ya Daudi)
1 Ee Mungu mtetezi wa haki yangu, unijibu niombapo.
Nilipokuwa katika shida, wewe ulinisaidia;
unionee huruma na kusikia sala yangu.
2 Jamani, mtaniharibia jina langu mpaka lini?
Mpaka lini mtapenda upuuzi na kusema uongo?
3 Jueni kuwa Mwenyezi-Mungu amejiteulia mwaminifu wake.
Mwenyezi-Mungu husikia kila ninapomwomba.
4 Tetemekeni kwa hofu na msitende dhambi;
tafakarini vitandani mwenu na kunyamaza.
5 Toeni tambiko zilizo sawa,
na kumtumainia Mwenyezi-Mungu.
6 Wengi husema: “Laiti tungepata tena fanaka!
Utuangalie kwa wema, ee Mwenyezi-Mungu!”
7 Lakini mimi umenijalia furaha kubwa moyoni,
kuliko ya hao walio na divai na ngano kwa wingi.
8 Nalala na kupata usingizi kwa amani;
ee Mwenyezi-Mungu, wewe peke yako waniweka salama.