Sala ya Mkimbizi
(Kwa Mwimbishaji. Utenzi wa Wakorahi)
1 Kama paa atamanivyo maji ya kijito,
ndivyo ninavyokutamani, ee Mungu wangu!
2 Naona kiu ya Mungu, kiu ya Mungu aliye hai.
Nitafika lini kwake na kuuona uso wake?
3 Machozi yamekuwa chakula changu mchana na usiku,
waliponiambia kila siku: “Yuko wapi Mungu Wako!”
4 Nakumbuka tena mambo haya
kwa majonzi moyoni mwangu:
Jinsi nilivyokwenda na umati wa watu,
nikawaongoza kwenda nyumbani kwa Mungu
wakipiga vigelegele vya shukrani;
umati wa watu wakifanya sherehe!
5 Mbona nasononeka hivyo moyoni?
Kwa nini nahangaika hivyo ndani mwangu?
Nitamtumainia Mungu,
maana nitamsifu tena
yeye aliye msaada wangu na Mungu wangu.
6 Nimesongwa na huzuni moyoni mwangu,
kwa hiyo ninakukumbuka wewe, ee Mungu,
kutoka katika eneo la Yordani,
kutoka mlima Hermoni na Mizari.
7 Nimeporomoshewa mafuriko ya maji
mafuriko ya maji yaja karibu
nayo yaita maporomoko mapya.
Mawimbi na mapigo yako yamenikumba.
8 Mwenyezi-Mungu atanijalia fadhili zake mchana;
nami nimwimbie wimbo wa sifa usiku,
nimwombe Mungu anipaye uhai.
9 Namwambia Mungu, mwamba wangu:
“Kwa nini umenisahau?
Yanini niende huko na huko nikiomboleza
kwa kudhulumiwa na adui yangu?”
10 Nimepondwa kwa matukano yao,
wanaponiuliza kila siku:
“Yuko wapi, Mungu wako!”
11 Mbona nasononeka hivyo moyoni?
Kwa nini nahangaika hivyo?
Nitamtumainia Mungu,
maana nitamsifu tena Mungu,
aliye msaada wangu na Mungu wangu.