Sala ya mkimbizi yaendelea
(Zaburi ya 42 yaendelea)
1 Onesha kuwa sina hatia ee Mungu;
utetee kisa changu dhidi ya watu wabaya;
uniokoe na watu waongo na waovu.
2 Nakimbilia usalama kwako ee Mungu;
kwa nini umenitupilia mbali?
Yanini niende huko na huko nikiomboleza
kwa kudhulumiwa na adui yangu?
3 Upeleke mwanga na ukweli wako viniongoze,
vinipeleke kwenye mlima wako mtakatifu,
kwenye makao yako.
4 Hapo, ee Mungu, nitakwenda madhabahuni pako;
nitakuja kwako, ee Mungu, furaha yangu kuu.
Nitakusifu kwa zeze, ee Mungu, Mungu wangu.
5 Mbona ninahuzunika hivyo moyoni?
Kwa nini nahangaika hivyo ndani mwangu?
Nitamtumainia Mungu,
nitamsifu tena
yeye aliye msaada wangu na Mungu wangu.