Mungu yuko upande wetu
(Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Wakorahi. Mtindo wa Alamothi)
1 Mungu ni kimbilio letu na nguvu yetu;
yeye ni msaada wetu daima wakati wa taabu.
2 Kwa hiyo hatutaogopa chochote,
dunia ijapoyeyuka
na milima kutikisika kutoka baharini;
3 hata kama bahari ikichafuka na kutisha,
na milima ikatetemeka kwa machafuko yake.
4 Kuna mto ambao maji yake hufurahisha mji wa Mungu,
makao matakatifu ya Mungu Mkuu.
5 Mungu yumo mjini humo, nao hauwezi kutikiswa;
Mungu ataupa msaada alfajiri na mapema.
6 Mataifa yaghadhibika na tawala zatikisika;
Mungu anguruma nayo dunia yayeyuka.
7 Mwenyezi-Mungu wa majeshi yu pamoja nasi,
Mungu wa Yakobo ni kimbilio letu.
8 Njoni mwone matendo ya Mwenyezi-Mungu;
oneni maajabu aliyoyafanya duniani.
9 Hukomesha vita popote duniani,
huvunjavunja pinde na mikuki,
nazo ngao huziteketeza.
10 Asema: “Nyamazeni na kujua kuwa mimi ni Mungu!
Mimi natukuka katika mataifa yote;
mimi natukuzwa ulimwenguni kote!”
11 Mwenyezi-Mungu wa majeshi yu pamoja nasi,
Mungu wa Yakobo ni kimbilio letu.