Mungu, Mfalme wa ulimwengu wote
(Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Wakorahi)
1 Enyi watu wote, pigeni makofi!
Msifuni Mungu kwa sauti za shangwe!
2 Maana Mwenyezi-Mungu, Mungu Mkuu, anatisha.
Yeye ni Mfalme mkuu wa ulimwengu wote.
3 Ametuwezesha kuwashinda watu wa mataifa,
ameyaweka mataifa chini ya mamlaka yetu.
4 Ametuchagulia nchi hii iwe urithi wetu,
ambayo ni fahari ya Yakobo anayempenda.
5 Mungu amepanda juu na vigelegele,
Mwenyezi-Mungu na sauti ya tarumbeta.
6 Mwimbieni Mungu sifa, mwimbieni!
Mwimbieni mfalme wetu sifa, mwimbieni!
7 Mwimbieni Mungu sifa kwa tenzi;
maana yeye ni mfalme wa ulimwengu wote.
8 Mungu anayatawala mataifa yote;
amekaa katika kiti chake cha enzi kitakatifu.
9 Viongozi wa watu wa mataifa wanakusanyika,
wanajiunga na watu wa Mungu wa Abrahamu,
maana nguvu zote duniani ni zake Mungu,
yeye ametukuka sana.